Ili
kuzaliana na kumpatia mfugaji faida, bata mzinga wanahitaji matunzo ya
hali ya juu. Kwa kawaida bata mzinga hula chakula kingi kuliko kuku. Bei
yake ni ghali zaidi. Kabla ya kuanza ufugaji wa bata mzinga ni lazima
kuhakikisha una chakula cha kutosha kwa sababu ulishaji wa ndege hawa
kadri wanavyokua huwa na gharama kubwa zaidi. Ni muhimu pia kujifunza
kwa undani na kufahamu namna ya kutunza vifaranga wa bata mzinga kwa
kuwa hufa kwa urahisi sana. Pia, unapaswa kujikita kutafuta soko kwa
sababu wanapokuwa ni vigumu kuwatunza kwa muda mrefu kutokana na ukubwa
wa gharama ya chakula.
Wafugaji
wachache kati ya wengi waliojaribu kuwafuga ndege hawa na kufanikiwa
hata kufikia malengo yao ni kutokana na kuzingatia lishe kamili. Pamoja
na hayo, wapo wafugaji ambao walishindwa kutokana na magonjwa pamoja na
gharama ya utunzaji.
Chakula
Chakula
cha bata mzinga hakina tofauti na cha kuku. Vifaranga wanahitaji kupata
lishe kamili yenye protini kwa wingi ili waweze kukua vizuri. Vifaranga
kwa siku za awali wanahitaji kiasi cha asilimia 27 ya protini mpaka
wanapofikia umri wa wiki sita. Baada ya hapo mfugaji anaweza kupunguza
hadi kufikia asilimia 18, na kuendelea hivyo hadi wanapokomaa. Kutokana
na gharama ya kununua chakula kuwa kubwa, unaweza kutumia reseheni
ifuatayo kwa ajili ya kutengeneza chakula cha bata mzinga wewe mwenyewe.
Mahitaji
• Mahindi 5kg (yasiyokuwa na dawa)
• Karanga 5kg
• Dagaa 5kg
• Mashudu 10kg
• Chokaa 5kg (chokaa inayotumika kwa lishe ya mifugo)
Namna ya kutengeneza chakula
Twanga
au saga pamoja kiasi cha kulainika kisha walishe vifaranga.
Mchanganyiko huu hutegemeana na wingi wa bata mzinga unaowafuga.
Hakikisha kila bata anapata chakula cha kutosha na chenye uwiano
ulioelekezwa. Pia waangalie mara kwa mara kuhakikisha wana chakula cha
kutosha.
Uhifadhi: Hifadhi chakula cha ziada kwenye mifuko au debe kisha weka sehemu isiyo na unyevu.
Kutaga
Bata
mzinga huanza kutaga anapofikisha umri wa mwaka mmoja. Ndege hawa wana
uwezo wa kutaga kati ya mayai 15 hadi 20 kwa mara ya kwanza na kisha
kuhatamia. Anapoendelea kukua huweza kutaga hadi mayai 30. Hii ni
kulingana na lishe nzuri atakayopatiwa.
Kuhatamia
Bata
mzinga anaweza kuhatamia mayai 17 hadi 20. Mayai hayo huhatamiwa kwa
siku 28 na huanza kuanguliwa vifaranga kwa muda wa siku 3, kuanzia siku
ya 28 hadi 31. Baada ya hapo mayai yaliyosalia bila kuanguliwa hutakiwa
kutupwa kwa kuwa hayatoanguliwa tena na hayafai kwa matumizi mengine.
Utunzaji wa vifaranga
Baada
ya vifaranga kuanguliwa, watenge na mama yao kwa kuwaweka kwenye banda
safi lisilopitisha baridi. Unaweza kuwawekea taa ya kandili au ya umeme
endapo upo kwenye sehemu unakopatikana.
Banda
Ni
vyema banda liwe limesakafiwa au banda la asili la udongo
usiotuhamisha maji. Pia, unaweza kutumia banda lenye mbao au mabanzi kwa
chini. Unaweza pia kutandaza maranda kwenye mabanda. Hakikisha kuta za
banda zimefunikwa vizuri ili kuwakinga dhidi ya baridi.
Maji
Kama
ilivyo ndege wengine, bata mzinga pia wanahitaji kupatiwa maji masafi
na ya kutosha wakati wote. Wawekee maji katika chombo ambacho
hawatamwaga na wanakifikia vizuri. Hakikisha maji hayamwagiki bandani
kwani kwa kufanya hivyo banda litachafuka na kukaribisha magonjwa kwa
urahisi. Ni vizuri kuwalisha bata mzinga vyakula vingine kama majani.
Majani husaidia kuwapatia protini: mfano; kunde, fiwi na aina nyingine
za majani jamii ya mikunde huhitajika zaidi kwa kiasi cha 25% hadi 30%.
Magonjwa
Bata
mzinga hushambuliwa na magonjwa kama taifodi, mafua na kuharisha damu.
Wanapougua ni rahisi kuambukiza kuku, bata na ndege wengine wanaofugwa
kwa haraka sana. Pia, ndege hawa husumbuliwa na viroboto wanaosababishwa
na uchafu wa banda hasa linapokuwa na vumbi.
Chanjo
Bata
mzinga wanatakiwa kupatiwa chanjo ya ndui (mara moja kila mwaka),
kideri (kila baada ya miezi mitatu), gumboro (kwa muda wa wiki tano -
ukiwapa jumatatu, basi unawapatia kila jumatatu ya wiki), na vitamini A
mara baada ya kuanguliwa.
No comments:
Post a Comment