Ili
kuzaliana na kumpatia mfugaji faida, bata mzinga wanahitaji matunzo ya
hali ya juu. Kwa kawaida bata mzinga hula chakula kingi kuliko kuku. Bei
yake ni ghali zaidi. Kabla ya kuanza ufugaji wa bata mzinga ni lazima
kuhakikisha una chakula cha kutosha kwa sababu ulishaji wa ndege hawa
kadri wanavyokua huwa na gharama kubwa zaidi. Ni muhimu pia kujifunza
kwa undani na kufahamu namna ya kutunza vifaranga wa bata mzinga kwa
kuwa hufa kwa urahisi sana. Pia, unapaswa kujikita kutafuta soko kwa
sababu wanapokuwa ni vigumu kuwatunza kwa muda mrefu kutokana na ukubwa
wa gharama ya chakula.
Wafugaji
wachache kati ya wengi waliojaribu kuwafuga ndege hawa na kufanikiwa
hata kufikia malengo yao ni kutokana na kuzingatia lishe kamili. Pamoja
na hayo, wapo wafugaji ambao walishindwa kutokana na magonjwa pamoja na
gharama ya utunzaji.
Chakula
Chakula
cha bata mzinga hakina tofauti na cha kuku. Vifaranga wanahitaji kupata
lishe kamili yenye protini kwa wingi ili waweze kukua vizuri. Vifaranga
kwa siku za awali wanahitaji kiasi cha asilimia 27 ya protini mpaka
wanapofikia umri wa wiki sita. Baada ya hapo mfugaji anaweza kupunguza
hadi kufikia asilimia 18, na kuendelea hivyo hadi wanapokomaa. Kutokana
na gharama ya kununua chakula kuwa kubwa, unaweza kutumia reseheni
ifuatayo kwa ajili ya kutengeneza chakula cha bata mzinga wewe mwenyewe.