Wafugaji wengi wa Tanzania wanafuga kuku wa kienyeji. Ndege hawa kwa
kawaida wanafugwa sehemu za vijijini ambapo wanaachiwa huru kuzurura.
Kuna uwezekano mkubwa sana wa kizazi kujirudia kwa kuwa jogoo anaweza
kumpanda mtetea ambaye alitokana naye, au kumpanda mtetea ambaye
wamezaliwa pamoja. Kuzaliana kwa namna hiyo kunasababisha matatizo
makubwa, ikiwa ni pamoja na kudumaa, kupunguza uzalishaji wa mayai, kuwa
na vifaranga dhaifu ambavyo ni rahisi kushambuliwa na magonjwa, na
mengineyo mengi yasiyokuwa ya kawaida. Ufugaji huru ambao una udhibiti
ni muhimu sana ili kuepuka kizazi kujirudia. Kuku wanaweza kuwekwa
kwenye makundi na kuachiwa kwa makundi ili kuzuia uwezekano wa kuzaliana
kwa kizazi kimoja.